(Shari) Mama Jamani asante!

Mama Jamani asante!
Nimekwenda wapi sipate, mama kama wewe ninao,
Umenilisha mkate, japo kwa nyumba ya mbao,
Umekaa siku fungate, nikinyonya tu mwanao,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,

Baba alipotuwacha, ulijawa na majonzi,
Kijiji kilipocheka, ulikolea masonzi,
Rafiki walitoroka, walikuita mlizi,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,

Mama cheka jamani, nione yako ufizi,
Kicheko kiso kifani, heri wakuone chizi,
Mama wewe wangu wani, nitakuombea kwa Razi,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,

Ringa tena ja tausi, ‘wakunyimi usingizi,
Wamekolea tetesi, hawakupi pumzi,
Usiwafanyie kesi, wao ni kama mkizi,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,

Wasema ulichangia, kwa abu kukata kamba,
Hawajui uliumia, zahanati ukiomba,
Jipe nguvu mama mia, Mola tu ni kama mwamba,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,
Jipodoe mama yangu, vya makogo we’ valia,
Mdomoni tia kizungu, ulisoma nakwambia,
Wanatamani mijungu, kwako watakusikia,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,

Wewe mfano mzuri, wewe ni mrembo pia,
Mola katia uturi, ndio ma’na wavutia,
Wasokutak’a mazuri, wasifanye ujutia,
Mama jamani asante, kwa kunilea mwanao,

Waadhi wa Malenga, Olunga Richard Karera.
Nairobi, Oktoba 13, 2011







Comments