Utangulizi
Tamthilia hii ya Mbivu zina Wenyewe… ni ya kimethali ambayo imetabdiliwa kisanaa ili kuleta dhana halisi ya ufisadi.
Huu ni ufundi wa mtunzi kwa nia ya kukoleza isitiari. Mojawapo tu ya mapochopocho kwenye tamthilia. Ufisadi ambao ndio ibra kuu kote duniani umerejelewa upya sasa.
Methali yenyewe ni Mvumilivu hula mbivu. Maana yake ni Mwenye stahamala atabwakia alichosubiria kwa muda fulani. Kisa na maana, ustahimilivu tu ndio kipengele.
Kubadili huko, kunaonyesha jinsi wafisadi wanavyoboronga haki za wanyonge. Japo, mnyonge msonge. Ikawa, Mvumilivu hula nunge na mbivu zina wenyewe.
Hii ni kama lugha ya kisirisiri amabayo inatumika tu na wanaoboronga haki hizo za kibinadamu, ili wasije wakajulikana – Rejista ya wafisadi.
Satua kuu la kitabu hiki ni kuhamasisha amani, upendo na utangamano. Swala lililotiwa kapuni haswa wakati wa vita na ghasia za baada ya uchaguzi, hapa nchini Kenya.
Tusiwahasisri wasio na hatia; wale ambao ni jirani zetu, ndugu zetu na wazazi wetu. Tuwapende, tuwatunze na tuishi nao abadi. Huo ndio ungwana, desturi za kina babu zetu isitoshe, mpangilio maalum uliowekwa na Maulana Rabi Msta.
Tuungane sisi wakenya, Afrika mashariki, Afrika yote na dunia nzima.
Enhee! Wenye kubuni wimbo wa Afrika mashariki, pokeeni shukrani zangu tumbitumbi manake, juzijuzi nilisimama tisti shabiku kinda kwenye kipupwe, miongoni mwa vijana wanaoeneza amani, kwa wimbo huo wenye mdunduizo wa kiafrika kweli. Ahsante! Yamkini, huko ndiko karama.
Kiswahili ni kitamu kushitadi asali!
Comments