Shairi la IDPS. (Wakimbizi wa ndani)


Mimi IDP mimi…

Kilio cha maskini, n’tamalizwa maskini
Ninaishi kihayawani, yamkini kambinini
Nimeliwa na kunguni, sina wa kunibaini
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

Vita vingetumaliza, tuliotiwa chonza
Moto uliwamaliza, wa kiambaa mi’ na waza
Wanasiasa wabeza, ahadi kutotimiza
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

Mwanzoni tulipendana, jirani kushikamana
Kwa dhiki kuinuana, kwa masonzi kupozana
Upendo hata kwa wana, waliotembeleana
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

Sasa wanachukiana, hawataki kuonana
Wanasiasa wakana, ‘wakupanga kupigana
Huko Hague ku’ namna, haki kweli itafana
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

Vijishamba tumekosa, waso IDP wamejitosa
Huko kambini kimakosa, au hata kwa kukosa
Ulingo hu wa siasa, utatutupa kwa kasa
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

Swala ni kupendana, tusibuni vita tena
Tungane ana kwa ana, na tujiinuwe tena
Mola anayetuona, atatupa nguvu tena
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

Vita hivyo viwe funzo, kwa vijana wetu sisi
N’ tusifanywe vibonzo, eti tupigane sisi
Kuungana kuwe mwanzo, tusikilize kasisi
Mimi IDP mimi, nitakuwa tajiri lini?

 Waadhi wa Malenga, Olunga Richard Karera.
Nakuru, Mei 2011

Comments